Jaji mkuu, Willy Mutunga amesalia na msimamo kuwa atastaafu mwezi Juni mwaka huu ili kuipa tume ya huduma kwa mahakama nafasi ya kutosha ili kusajili jaji mkuu mpya.
Akijibu maombi ya baadhi ya wanasiasa haswaa kutoka mrengo wa CORD ya kumtaka abadili nia yake ya kustaafu hivi karibuni, Mutunga alisisitiza kuwa hatabadili uamuzi wake wa kustaafu.
Mutunga ambaye aliingia ofisini Juni 20,2011 alisema kuwa ameamua kuondoka ofisini mapema ili kuiokoa nchi ya Kenya kutokana na kile alichokitaja kama ushawishi mkali utakaoleta utatanishi katika kumchagua mrithi wake.
‘‘Uchaguzi wa Jaji mkuu sio suala la kufanywa kwa siku moja, ni suala linalochukua muda mrefu kwani kuna kushirikishwa kwa umma ushawishi kutoka kwa bunge na mahakama,’’ alisema Mutunga.
‘‘Suala hilo halifai kuharakishwa. Ndio maana nimeamua kutoka ofisini mapema,’’ alisema Mutunga.
Mutunga pia alisema kuwa kuondoka kwake mapema kutamwezesha mrithi wake kuzoea majukumu yake kwa haraka baada ya kuchaguliwa huku akisisitiza kuwa jaji mwingine hawezi chaguliwa mwingine akiwa ofisini.
Hapo awali, wabunge David Ochieng (Ugenya) na Omondi Muluan (Alego-Usonga), walimwagiza Mutunga kutoondoka ofisini kabla ya mizozo inayoikumba mahakama kutatuliwa. Ochieng alimwagiza Mutunga kustaafu baada ya visa vya ufisadi vinavyokumba mahakama kutatuliwa.