Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mwenyekiti wa shirika la kitaifa la kukabiliana na mihadarati na pombe Nacada John Mututho amesema kaunti hazistahili kujifaidi kutokana na fedha zinazokusanywa kutoka kwa leseni za kuuza pombe.

Akizungumza siku ya Ijumaa kupitia mahojiano kwenye njia ya simu, Mututho alisema kuwa fedha hizo zinazokusanywa baada ya leseni kutolewa kwa kampuni za kutengeza pombe na maeneo ya kuuzia vileo zafaa kutumika kutengeneza makao ya kuwasaidia waathiriwa wa pombe haramu na pia kusimamia matibabu ya waathiriwa hao.

“Fedha zote ambazo hutoka kwenye leseni zafaa kutumika kwa maswala ya kuwashughulikia na kurekebisha mienedo walioathiriwa na pombe. Huwezi chukua yale mapato ya kufungua vilabu na kuyatumia kwa mambo mengine,” alisema Mututho.

Aidha, mwenyekiti huyo alisema ingawa kampeni ya hivi majuzi ya kukabiliana na uuzaji wa pombe haramu ilikamilika, misako ingali inaendelezwa kwenye sehemu mbalimbali za kenya na yeyote atakayepatikana na hatia hiyo huenda akatozwa faini ya shilingi millioni kumi au kifungu cha miaka mitano gerezani.

“Mtu kama hajui asome sheria ya Mututho kipengee cha 38 kinachohusiana na pombe haramu. Utafungwa takriban miaka mitano au utalipa shilingi milioni kumi,” aliongeza Mututho.

Wakati huo huo, Mututho alisema kuwa maafisa wa polisi na machifu pia wameshirikishwa kwenye shirika hilo la Nacada na kutokana na hilo, shirika hilo linawakilishwa hadi vijijini.