Wamiliki wa magari kote nchini wameonywa kuwa magari yao yakipatika yakisafirisha dawa za kulevya yatachukuliwa na kumilikiwa na Serikali.
Akiongea siku ya Ijumaa katika hitimisho la mafunzo jinsi ya kupambana na madawa ya kulevya katika Chuo Kikuu cha Kisii, mwenyekiti wa Tume ya kupambana na dawa za kulevya almaarufu NACADA John Mututho aliwaonya wamiliki wa magari kote nchini kutoruhusu gari zao kusafirisha dawa za kulevya na yakipatikana yatamilikiwa na Serikali.
“Gari lolote litakalo patikana likisafirisha dawa ya kulevya litachukuliwa na kumilikiwa na Serikali na mwenye gari hilo pia achukuliwa hatua ya kisheria,” alihoji Mututho.
Kwa mujibu wa Mututho, magari mengi hutumiwa kusafirisha dawa za kulve ambazo zimeathiri maisha ya watu wengi, haswa ya vijana.
Tume ya kupambana na dawa za kulevya kupitia mwenyekiti wao wamechukua hatua hiyo kufuatia utafiti ulioonyesha kuwa kuna baadhi ya watu wanao kodi magari na kutumia kwa kusafirisha dawa hizo.
“Tunaamini kuwa tukifanya hivyo viwango vya dawa za kulevya vitapungua haswa kusafirishwa kutoka eneo moja hadi nyingine,” aliongezea Mututho.
Vile vile Mututho aliomba kuwa wale wameathirika na dawa za kulevya katika jamii wapewa ushauri na mafunzo muhimu jinsi ya kujiepusha na dawa hizo.