Mwenyekiti wa mamlaka ya Nacada aimeitaka serikali kubuni kikosi maalum cha kukabiliana na pombe haramu na dawa za kulevya.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Akizungumza katika mahojiano na mwandishi huyu kupitia njia ya simu siku ya Jumatatu, Bwana John Mututho alisema kikosi hicho maalum kitakuwa na vifaa maalum vya kukabiliana na wahusika kwa usaidizi wa polisi wa kawaida.

“Serikali imejaribu kukabiliana na pombe haramu na dawa za kulevya lakini bado juhudi zao hazijafaulu ipasavyo,” alisema Mututho.

Mututho, ambaye ni mbunge wa zamani wa Naivasha, alisema kuwa mamlaka tofauti nchini kama vile KRA, na NTSA huwa na maafisa spesheli ambao husaidia mamlaka hizo kutekeleza juhudi zao.

Mututho alisema kuwa ni jambo la kuhuzunisha kuona vijana katika maeneo ya Molo, Elburgon, Gatundu Kusini, na Mombasa wakiathirika na matumizi ya pombe haramu na mihadarati.

“Hali iliyopo katika maeneo ya Molo, Gatundu na Pwani mwa Kenya inahuzunisha. Hiyo ndiyo sababu tunaitaka serikali kuhakikisha kuwa sheria za Mututho zinatiliwa maanani. Pia tunapendekeza kubuniwa kwa kikosi spesheli chenye magari na vifaa maalum vya kukabiliana na janga hili,” alisema Mututho.