Mwenyekiti wa shirika la Nacada John Mututho ametaka mmliki wa baa ambayo vijana wanane walibugia vileo kabla ya kuhusiaka katika ajali katika mkesha wa mwaka mpya ashtakiwe kwa mauwaji.
Mututho aliashiria kwamba leseni ya baa hiyo iliyoko kwenye barabara kuu ya Nakuru-Nairobi itafutiliwa mbali baada ya maafisa wa polisi kukamilisha uchunguzi wao.
Akizungumza kwenye eneo la Salgaa wakati wa shughuli ya kuhamasisha waendeshaji wa malori siku ya Jumatatu, Mututho alisema kwamba wakati umewadia kwa wanaowauzia watoto vileo kukabiliwa kisheria.
Alisema kwamba kundi la maafisa wa Nacada wakishirikiana na maafisa wa polisi litakuwa likizuru maeneo ya burudani kuhakikisha kwamba ni watu wazima tu wanaobugia vileo.
Kwa muujibu wake, tayari amezungumza na baadhi ya wabunge kuhusiana na hitaji ya kubuni sheria inayohusiana na umri unaoruhusiwa kwa watu kuanza kunywa pombe kutoka miaka 18 hadi miaka 21.
Kando na hayo, Mututho alisema kuwa iwapo bunge litapitisha mswada mmoja ulio bungeni kuwa sheria, leseni ya dereva yeyote yule atakayesababisha ajali itafutiliwa mbali kabisa.
Mututho alisema kuwa ingawa idadi ya ajali ambazo zimetokana na madereva waliokuwa walevi msimu wa krismamsi ni chache, kuna kesi nne zilizoripotiwa za waliowauzia watoto pombe.
Kwa upande mwingine, amehimiza serikali ya kaunti ya Nakuru kuchunguza kwa makini maeneo yanayouza pombe kabla ya kutoa leseni.