Share news tips with us here at Hivisasa

Mwenyekiti wa bodi ya kudhibiti pombe na dawa za kulevya John Mututho ametishia kuwahamasisha wapiga kura kutowachagua wabunge ambao hawataunga mkono marekebisho ya sheria ili kubadilisha kipengele kinachoruhusu mtu kunywa pombe, kutoka miaka 18 hadi 21.

Mututho alisema kwamba uchunguzi umeonyesha kuwa aslimia 15 na aslimia 40 ya kansa ya matiti na koo mtawalia, husababishwa na unywaji wa pombe haswa vileo vikali vinavyotengenezwa karne hii ya 21.

Mututho alionya kwamba kama umri huo hautasongeshwa hadi miaka 21, basi kizazi kipya kimo hatarini ya kupatwa na kansa katika umri mchanga.

Akiongea Jumanne kwenye kanisa katoliki la Mtakatifu Lwanga huko Njoro kaunti ya Nakuru, baada ya kuhudhuria ibada ya mazishi ya vijana watano walioaga kwenye ajali ya barabarani eneo la Salgaa kwenye barabara kuu ya Nakuru-Eldoret mkesha wa mwaka mpya, Mututho aliwataka wabunge kufanyia sheria mabadiliko hayo ili kuokoa kizazi kipya.

“Ninapongeza sana vilabu vya jiji la Nairobi ambavyo vimekubali kutouzia yeyote ambaye hajafikisha umri wa miaka 21 pombe. Mataifa mengine kama Marekani yamefanikiwa kuendeleza sheria hiyo, na Kenya inafaa kuiga mfano huo,” alisema Mututho.