Mwenyekiti wa mamlaka ya kupambana na pombe haramu na dawa za kulevya (NACADA) John Mututho, ameonya wanaoendeleza biashara ya pombe haramu wilayani Molo huku akisema mamlaka hiyo iko tayari kufanya oparesheni ya wiki moja katika eneo hilo ili kupambana na biashara hiyo haramu.
Mututho amesema idadi ya watu ambao wamepoteza maisha yao baada ya kubugia pombe haramu inaendelea kuongezeka nchini licha ya serikali kufanya oparesheni ya kumwaga pombe hiyo mwaka jana.
Mwenyekiti huyo amesema bado amri ya rais Kenyatta ya kumwaga pombe hiyo hatari iko imara huku akisema watakaopatikana na hatia watachukuliwa hatua kali za kisheria.
“Hakuna nafasi kwa wapishi katika serikali ya rais Uhuru Kenyatta, ninarudia tena sina haja ya kwenda kuitisha msaada kutoka kwa katibu wa kudumu katika wizara wa usalama wa ndani Karanja Kibicho ama rais, nina mamlaka ya kuwachukulia hatua wanaokiuka sheria za mivinyo,” alisema Bw Mututho akiwahutubia wakaazi mjini Molo Jumanne ikiwa ni siku yake ya pili mjini humo.