Aliyekuwa mbunge wa Naivasha John Mututho ameutaka uongozi wa kaunti ya Nakuru kukoma kumchafulia jina na badala yake wazingatie maswala muhimu ya maendeleo ya kaunti.
Akizungumza siku ya Jumanne, Mututho alikashifu madai ya gavana Kinuthia Mbugua na mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri ya kutilia shaka mchango wake wa shilingi elfu mia tatu za kusaidia gharama ya matibabu ya mwenyekiti wa maendeleo ya wanawake Kaunti Ya Nakuru aliyepata ajali mwaka jana.
Kutokana na hilo, Mututho alisema kuwa yuko tayari kukabiliana na gavana Mbugua wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2017.
Aidha, Mututho anadai kuwa gavana Mbugua hana nafasi ya kushinda katika uchaguzi mkuu ujao kwani amefeli kutekeleza ahadi za kimsingi ikiwemo miundo misingi mingi ya kuwasaidia wakaazi wa kaunti.
Wakati huo huo, Mututho ambaye ni mwenyekiti wa mamlaka ya kukabiliana na matumizi ya pombe na dawa za kulevya humu nchini NACADA alisema, badala ya Gavana Mbugua kutilia shaka mchango wake na kutumia jukwaa hilo kukashifu wengine, angetumia uwezo alionao kusaidia kujua ni nani anayewaua makahaba mjini Nakuru pamoja na maeneo mengine ya kaunti ya Nakuru.