Mamlaka ya kupambana na pombe haramu na dawa za kulevya nchini Nacada imeitaka serikali kuunda kikosi maalum cha kukabiliana na pombe haramu na dawa za kulevya.
Mwenyekiti wa Nacada John Mututho amesema “serikali imejaribu kukabiliana na pombe haramu na dawa za kulevya” lakini bado juhudi zao hazijafaulu ipasavyo.
Akizungumza kwa njia ya kipekee na mwandishi huyu kwa simu, Mututho ambaye ni Mbunge wa zamani wa Naivasha, alisema kikosi hicho maalum kitakuwa na vifaa maalum vya kukabiliana na wahusika kwa usaidizi wa polisi wa kawaida.
“Kila pahali kama ni KRA, Kenya Railways, NTSA wao wako na maafisa spesheli, na hivyo ndivyo tunataka kwa Nacada,” akasema.
Mututho alihuzunikia pombe na dawa ambazo zinaendelea kutumiwa na vijana haswa katika eneo bunge la Molo, Elburgon, Gatundu Kusini, na eneo la Mombasa.
“Hali iliyopo katika upande wa Molo vijiji vya Moto na Chandera, Gatundu na Pwani mwa Kenya inahuzunisha. Ndio maana nataka serikali iangalie sheria za Mututho na pia NACADA ACT na itimize mahitaji yake ya kuunda kikosi spesheli chenye magari na vifaa maalum,” alisema Mututho.