Muungano wa waathiriwa wa ghasia za uchaguzi mkuu wa 2007-08 ambao wanadai kutelekezwa na serikali Jumamosi walitoa makataa ya hadi Mei wawe wamelipwa fidia na wapewe makao maalum, la sivyo wataandamana.
Wamesema kuwa serikali imekuwa ikiwahadaa Wakenya kuwa imetia bidii katika kuwapa ardhi na fidia il hali bado kuna takriban waathiriwa 200,000 ambao wamesahaulika.
Kwa mujibu wa msemaji wao kutoka Kaunti za Nakuru na Nyandarua Bw Muigai Kang’au, hofu yao kuu ni kuwa kusambaratika kwa kesi za washukiwa wa ghasia hizo katika mahakama ya ICC kutaifanya serikali kuwasahau.
“Tuko katika njia panda na kwa sasa ikiwa hatutang’ang’ania kupata haki, basi tusahau milele kuwahi kushughulikiwa,” alisema.
Bw Kang’au alisema kuwa kufikia sasa kuna ishara tosha za mwanzo wa kusahaulika na serikali kwa kuwa “tayari tumeandaa mikutano kadhaa na wadau wa kutupa fidia na makao lakini jinsi ilivyoanza kuwa wazi kesi hizo zingetupwa, serikali ilianza kutuhepa
Alisema mwanzoni mwa 2016 wawakilishi wa waathiriwa hao waliandaa mkutano jijini Nairobi na waziri mpya wa ugatuzi na mipango ya kitaifa Bw Mwangi Kiunjuri ambapo waliafikiana kuhusu njia mwafaka za kuharakisha zoezi hilo la kuwatunza.
“Lakini tangu wakati kesi za mwisho katika mahakama ya ICC zilizowahusisha Naibu wa rais Bw William Ruto na aliyekuwa mtangazaji Joshua arap Sang' zilipoanza kuonyesha dalili za kusambaratika, Bw Kiunjuri alianza kutuhepa,” alisema.
Bw Kang'au alikuwa akizungumza mjini Nakuru.