Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Muungano wa vyama vya akiba na mikopo nchini KUSCO umeelezea hofu ya kupata hasara kubwa baada ya kusimamishwa kwa mishahara ya walimu.

Akizungumza wakati wa kongamano la kibiashara na wadau wa vyama hivyo mjini Mombasa siku ya Jumamosi, Mkurugenzi mkuu wa muungano huo George Ototo alisema kwamba tayari vyama 26 vinakabiliwa na uhaba wa fedha.

Bw Ototo alisema hasara hiyo imetokana na serikali kuu pamoja na tume ya kuajiri walimu nchini TSC kutowalipa walimu mishahara yao hususan ule wa mwezi wa Septemba.

Aidha, alisema vyama hivyo vinadai zaidi ya bilioni 2.1 za mikopo kutoka kwa walimu kote nchini waliyochukua mikopo kwa vyama vya akiba na mikopo ili kutekeleza miradi mbalimbali za kimaendelea mashinani.

“Tumeamua kuchukua jukumu la kusitisha mikopo kwa walimu wote kote nchini baada ya kupata hasara kubwa ya malimbikizi ya madeni tunayowadai walimu ambao bado hawajalipa kutokana na kukosa mishahara yao," alisema Bw Ototo.

Naye mkurugenzi wa chama cha akiba na mikopo cha Imarika George Masha alisema kwamba kwa sasa wamesitisha mikopo kwa walimu kote nchini ili kuona kwamba wanakabili hasara hiyo.

“Tunahofikia huenda chama chetu kikasambaratika iwapo madeni tunayodai yatakosa kulipwa kwa wakati kwani hatua hii inadidimiza uchumi wa taifa hili na maendeleo ya wakazi mashinani," alisema Bw Masha.

Mchakato huyo imejiri baada ya walimu kushiriki mgomo wa kitaifa wakishiniza serikali kuwalipa mishahara yao pamoja na marupurupu ya asilimia 50 hadi 60 hatua ambayo ilipelekea serikali kutowalipa mishahara yao ya mwezi wa Septemba.