Muungano wa wabunge wa Pwani umetakiwa kusitisha malumbano ya kila mara kufuatia kubadilishwa kwa viongozi wa muungano huo na badala yake kuwaunganisha wapwani.
Mwenyekiti wa Chama cha Uzalenzo nchini CCU, Maur Bwanamaka Abdallah amesema kuwa muungano huo unafaa kuonyesha kile walichowafanyia wapwani hasa katika kupigania ardhi za wapwani, muundo msingi, elimu na usalama badala ya wao kuzozana kuhusu uongozi wa muungano huo.
Amesema kuwa wapwani kwa sasa wanachohitaji ni kuona manufaa ya muungano huo katika kipindi ambacho muungano huo uliundwa, huku akisema kuwa huenda ikawa muungano huo ni wa kisiasa na wala hauna malengo yoyote ya kuwasaidia wapwani.
"Tunataka kuona muungano wa wabunge wa pwani kufanyia wakazi mambo muhimu hasa swala kusitisha unyakuzi wa ardhi, usalama, elimu na maswala mengine muhimu na wala sio kutumia muungano huo kujipigia debe kisiasa," alisema Bwanamaka siku ya Jumatatu mjini Mombasa.
Kiongozi huyo amedai kuwa iwapo muungano huo wa wabunge wapwani hautakua na msimamo dhabiti, basi itakuwa kiegezo cha baadhi ya viongozi kujipigia debe kisiasa kupitia kwa muungano huo kinyume na matarajio ya wapwani.