Huku muungano wa wafanyakazi wa bandari ukitarajiwa kuandaa uchaguzi wa kuteua viongozi wao kwenye awamu nyingine, baadhi ya wanaowania viti hivyo pamoja na washika dau kwenye muungano huo wametoa hofu kuwa huenda upande unaongozwa na katibu wa sasa Simon Sang ukaiba kura na kunyakua ushindi.

Share news tips with us here at Hivisasa

Wakizungumza siku ya Jumanne, wafanyikazi hao walisema sharti katibu wa sasa afuate sheria iwapo atashindwa na mojawapo wa wapinzani wake.

Wafanyikazi hao wa bandari kupitia kwa kiongozi wao Geofrey Mareko, walisema kuwa wana wasiwasi kuwa huenda usimamizi wa sasa wakatumia njia za mkato na kujipatia ushindi kwenye kura hizo.

Wengi wa wafanyakazi ambao waliongea na mwandishi huyu walisema kuwa kunahitajika mabadiliko makubwa ya uongozi pamoja na mazingira ya kufanya kazi kwenye bandari hiyo.

Aidha, walisema kuwa wakati umefika kwa viongozi wa zamani kuwapa nafasi viongozi wengine, ili kuleta uongozi tofauti kwenye sekta hiyo.

Baadhi ya wanaotarajiwa kuwania uongozi na nyadhifa mbali mbali kwenye muungano huo wa wafanyakazi ni pamoja na Bakari Bweta, Abdalla Randan, Wara Katana, miongoni mwa wengine.

Hii itakuwa awamu ya tatu kwa katibu mkuu wa sasa Simon Sang, ambaye ameandaa maandamano mara mara kupigania haki za wafanyakazi hao kuwawania nyadhifa hiyo ya uongozi.