Muungano wa maendeleo ya wanawake nchini umejitokeza na kutoa pongezi kwa Naibu Rais William Ruto baada ya kesi iliyokuwa ikimkabili katika mahakama ya ICC kufutiliwa mbali.
Wanawake hao wamesema hatua hiyo itampa fursa naibu rais kutekeleza majukumu yake bila pingamizi zozote tofauti na hapo awali.
Akiongea katika hafla iliyowaleta pamoja wanawake kutoka kaunti sita za Pwani mjini Mombasa siku ya Jumatano, mwenyekiti wa kitaifa wa muungano huo Rahab Mwikali alisema kuwa maombi ya Wakenya yalisikika.
“Tulingoja sana kwa muda mrefu kama Wakenya na hatimaye haki imepatikana kwa sababu hata nchi hii pia ilikuwa imebeba mzigo mzito sana,” alisema Bi Mwikali.
Hata hivyo, Mwikali aliongeza kuwa serikali inafaa kuchukua nafasi hii na kuwafidia waathiriwa wa ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007 ambao bado wanakumbwa na changamoto ya umaskini.
Alisema hatua hiyo itahakikisha waathiriwa hao wamepata haki yao hata baada ya kupitia hali ngumu ya maisha tangu vita hivyo vilipokamilika miaka tisa iliyopita.
“Ningependa muungano wetu kuhusishwa katika kuhakikisha hakuna mtu hata mmoja aliyeathirika wakati wa vita anaachwa akiteseka. Huu ni ujumbe ambao natuma hadi kwa rais na naibu wake,” aliongeza Mwikali.
Wakati huo huo, washiriki wa muungano wa maendeleo ya wanawake kanda ya Pwani walisema kuwa watakuwa katika msafara kwenda kuhudhuria hafla ya kusherekea uamuzi huo mjini Nakuru siku ya Jumamosi.
Sherehe hizo ambazo zinazotarajiwa kuhudhuriwa na Rais Uhuru Kenyata pamoja na viongozi wengine serikalini zitafanyika katika uwanja wa Afraha.