Mwenyekiti wa muungano wa wazazi nchini Musau Ndunda amepinga vikali pendekezo la katibu mkuu wa chama cha Knut Wilson Sossion, la kutaka wanafunzi waruhusiwe kutumia simu shuleni.
Kwenye mahojiano kwa njia ya simu na mwandishi huyu siku ya Alhamisi, Ndunda alielezea kushangazwa na pendekezo hilo, kwa kusema kuwa litachangia kuwapotosha wanafunzi kimaadili, hasa kutokana na matumizi wa mitandao ya kijamii.
“Kwa niaba ya wazazi, nataka kusema hatutakubali wala kuwaruhusu wanafunzi kwenda na simu shuleni. Sossion anafaa kufikiria mara mbili kabla kutoa mapendekezo kama haya. Hii ni kuwapotosha wanafunzi,” alisema Ndunda.
Aidha, Ndunda alisema kuwa simu zitachangia ongezeko la visa vya utovu wa nidhamu shuleni, na hata kueneza wizi wa mitihani ambao umekuwa changamoto kuu nchini.
“Tumekuwa tukilalama kuwa simu inatumika na wanafunzi na hata baadhi ya walimu kusambaza mitahani kupitia mitandao mbalimbali kama vile Facebook na WhatsApp. Iweje leo hii mtu apendekeze simu iruhusiwe shuleni?” alisema Ndunda.
Kauli ya Ndunda iliungwa mkono na wazazi waliozungumza na mwandishi huyu, walioonekana kukerwa na pendekezo hilo.
Siku ya Jumatano, mwenyekiti wa chama cha Knut Wilson Sossion alinukuliwa kwenye vyombo vya habari akipendekeza wanafunzi kuruhusiwa kutumia simu shuleni hasa wakati wa somo la kiteknologia.