Mvua kubwailiyonyesha katika kaunti ya Nakuru leo Alhamisi ilikatiza kwa ghafla mkutano wa gavana Kinuthia Mbugua katika kituo cha kibiashara cha Bahati.
Gavana Mbugua alikuwa amezuru wadi ya Bahati kufungua miradi kadhaa ya maendeleo ambayo imefadhiliwa na serikali yake kwenye lokesheni saba za wadi hiyo tangia kuingia mamlakani, kisha ahutubie wakazi katika uwanja wa mpira wa kituo hicho.
Hata hivyo baada ya kufungua miradi hiyo ikiwemo ua la soko jipya la Bahati, miradi ya maji na hospitali, wanenaji kadhaa akiwemo mwakilishi wa wadi hiyo Peter Nderitu walipewa nafasi ya kuzungumza lakini dakika chache baada ya gavana huyo kuchukua kipaza sauti, mvua kubwa ikamwagika na kukatiza hotuba yake.
Walinzi wa gavana huyo, wakazi na viongozi wote waling’ang’ana kushikilia hema zilizokuwa zimeezekwa ili zisibebwe na upepo mkali ulioandamana na mvua hiyo.
Hayo yote yakijiri gavana Mbugua alidinda kuingia kwenye gari lake baada ya walinzi na dereva wake kulileta karibu naye kumwondolea gadhabu ya mvua, huku akionekana kuwaashiria waondoe gari karibu na wakazi.
Viti na baadhi ya hema ziliangushwa na mvua hiyo huku umati ukilazimika kufumukana. Mwakilishi wa wadi hiyo Peter Nderitu Mwangi alisema kwamba mvua ilikuwa baraka huku akipongeza serikali ya Kinuthia Mbugua kutokana na kujituma kwake kufanya maendeleo.
Hata hivyo mvua ilipopungua baada ya dakika 30 hivi, gavana huyo aliahirisha mkutano huo hadi mwezi ujao, ambapo anatarajiwa kukutana na wakazi hao wa Bahati tena.
“Siku ya leo nilikuwa nimepanga kuwa nanyi, lakini mvua ambayo tumekuwa tukiomba ije haijatupa nafasi. Mwezi ujao tutapanga kukutana nayi tutimize yale ambayo hatukutimiza leo” akasema gavana Mbugua na hatimaye akaondoka.