Share news tips with us here at Hivisasa

Mvulana mmoja mwenye umri wa miaka 12 alijitoa uhai kwa kujitia kitanzi kwa kutumia neti siku ya Jumatatu katika kijiji cha Esiagi, wilayani Masaba Kaskazini Kaunti ya Nyamira.

Akithibitisha kisa hicho, naibu wa chifu wa kata ndogo ya Nyankoba, Erik Marando, alisema kuwa mwili wa marehemu Isaac Nyagaka ambaye alikuwa mwanafunzi wa darasa la tatu katika shule ya msingi ya Chitago, wilayani humo, ulipatikana umening’inia mtini nje ya nyumba yao.

“Wakati wa tukio hilo hamna aliyekuwa nyumbani na aliyekuwa wa kwanza kufika nyumbani ni nduguye mdogo aliyekumbana na mwili wake ukining’inia mtini na kupiga kamsa. Wanakijiji walifika hapo na kuwaita maafisa wa polisi,” alisema Marando.

Aidha, chifu huyo alisema kuwa haijajulikana kilichompelekea marehemu kuchukua hatua hiyo akiongezea kuwa maafisa wa polisi wameanzisha uchunguzi.

“Maafisa wa polisi walifika katika pahala pa tukio na kuchukua maiti ya marehemu hadi kwenye hifadhi ya maiti ya hospitali ya Gucha mjini Keroka na uchunguzi umeanzishwa,” alisema Marando.