P { margin-bottom: 0.08in; }

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

P { margin-bottom: 0.08in; }

Mvulana mwenye umri wa miaka 13 alifariki mnamo Ijumaa katika kijiji cha Kambaa kwenye eneobunge la Lari baada ya kuangukiwa na mti akitema kuni.

Michael Mwangi alikuwa ameenda kwenye msitu wa Kiriita kutema kuni wakati aliangukiwa na mti na kufa papo hapo.

Waliofika mahali pa tukio walisema kuwa mti huo ulikuwa umeoza na hivyo basi kwa urahisi uliangukia mvulana huyo pasipo yeye kujua hatari iliyokuwa pale.

Mwangi alikuwa mwanafunzi katika shule ya msingi ya Kiriita.

Polisi wakishirikiana na wakazi walibeba mwili wa mvulana huyo kwa kilomita nne kutoka kwa msitu huo kwani hakuna barabara ambayo gari lingetumia kuingia hadi pale kubeba maiti hiyo.

Babake marehemu, Peter Kimani, alihuzunika na kifo cha mwanawe ambaye alisema ni mwenye bidii na mtiifu kwa wakubwa wake.

Kimani alisema kuwa pengine walimu wangekuwa shuleni mtoto wake hangekufa.

“Serikali inastahili kuona kuwa mgomo wa walimu umeisha kwani pengine mtoto wangu hangekuwa msituni akiokota kumi na kupatwa na janga hilo, angekuwa darasani akisoma,” alisema.

Majirani walihuzunika kwa kifo hicho cha mvulana mchanga.

John Mburu, mmoja wa wakazi, alisema, “Hapa Lari kuna misitu mingi sana kukilinganishwa na maeneo mengine ya Kiambu na tunaomba serikali kuangalia misitu na kuhakikisha hakuna hatari misituni kama ambayo imetupata leo.”

Mkuu wa polisi eneo hilo Alfred Makoma alisema kuwa mwili wa marehemu ulihifadhiwa katika chumba cha maiti cha Uplands hapo Nyambari, Lari.

“Tutaangalia mti ambao unasemekana kusababisha kifo hiki na kutoa ripoti kamili kuhusu kifo cha Mwangi,” alisema OCPD Makoma.