Mvulana mmoja mwenye umri wa miaka 14 alijitia kitanzi siku ya Jumanne katika kijiji cha Itongo Sengera, Wilayani Masaba Kaskazini, Kaunti ya Nyamira.
Akithibitisha kisa hicho, naibu wa chifu katika kata ndogo ya Biticha Richard Nyang’au, alisema kuwa marehemu Samuel Ogero, ambaye ni mwanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya msingi ya Itongo Sengera alimwambia nduguye mdogo ambaye walikuwa wamelala pamoja kuwa atakapokufa amlindie vizuri kuku wake.
Nyang’au alisema kuwa nduguye mdogo alipoamka alipata mwili wa marehemu ukining’inia paani mwa chumba hicho na kupiga kamsa.
“Kulingana na nduguye mdogo, walipokuwa wakijiandaa kulala, marehemu alimwambia kuwa amlindie kuku wake vizuri lakini hakujua sababu ya ujumbe huo hadi alipompata Ogero akiwa ameaga dunia,” alisema Nyang’au.
Aidha, chifu huyo alisema kuwa sababu ya kijana huyo kujitoa uhai haijabainika, akiongezea kuwa maafisa wa polisi wameanzisha uchunguzi.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Chumba cha kuhifadhi maiti Cha Gucha mjini Keroka.
“Maafisa wa polisi walifika katika boma hiyo na kuuchukua mwili wa marehemu, huku uchunguzi ukianza,” alisema Nyang’au.