Share news tips with us here at Hivisasa

Gavana wa kaunti ya Kwale Salim Mvurya amefanya kikao cha faragha na viongozi wa Shirika la Huduma za Feri nchini kutathmini jinsi ya kuimarisha shughuli za uchukuzi katika kivuko cha feri cha Likoni.

Kikao hicho kilijadili masuala mhimi ikiwemo jinsi ya kuimarisha shughuli za uchukuzi katika kivuko cha feri cha Likoni, uimarishaji wa sekta ya utalii, uchumi na biashara baina ya maeneo ya Kisiwani Mombasa na Pwani kusini.

Gavana Mvurya, ambaye pia ni naibu mwenyekiti wa baraza la magavana nchini amesema kuwa katika kikao hicho, waliafikiana kujengwa kwa eneo la kuegesha magari ya uchukuzi wa mzigo wakati wa kusubiri feri kuvuka ng’ambo ya pili ili kuzuia kushuhudiwa majanga.

Akiongea na wanahabari baada ya mkutano huo katika afisi za shirika la huduma za feri nchini siku ya Jumanne mjini Mombasa, Gavana Mvurya alisema kuwa katika siku za usoni, wanatarajia kununua meli ya abiria ambayo itasadia katika masuala ya utalii ikiwa kusafirisha watalii kutoka kisiwani Mombasa hadi kusini mwa Pwani hasa maeneo ya Diani na Ukunda.

"Tunafanya mzungumzo mhimu na tunatarajia kuona mabadiliko katika kivuko cha feri cha Likoni hasa katika masuala ya uchukuzi, utalii, uchumi na biashara na yale tuliyoyajadili yana umuhimu mkubwa kwa wakazi wa Pwani kwa jumla na wale wanatumia kivuko cha feri cha Likoni," alisema Gavana Mvurya.

Mvurya ameahidi kukamilika kwa malengo waliyoafikiana kwa kiwango kikubwa shughuli za uchukuzi na masuala mengine katika kivuko cha feri cha Likoni yataimarishwa zaidi hasa kupungua kwa msongamano wa mara kwa mara.