Gavana wa Kaunti ya Kwale Salim Mvurya pamoja na naibu wake Fatuma Achani wamemshutumu Seneta Boy Juma Boy kwa kueneza uvumi kuwa Mvurya alihamia mrengo wa Jubilee baada ya kunyakua kipande cha ardhi katika eneo bunge la Lunga Lunga.
Wakizungumza na waandishi wa habari katika eneo la Diani, viongozi hao walisema kuwa uvumi huo huana ukweli wowote.
Walisema kuwa madai hayo hayana msingi kwani unyakuzi wa ardhi hautekelezwi na chama, ila mtu binafsi, huku wakiongeza kuwa dhulma za ardhi katika eneo la Pwani ziwekuwepo tangu zamani.
Kwa upande wake, Bi Achani alisema kuwa serikali ya Jubilee haipaswi kulaumiwa kwa wizi wa mashamba katika eneo la Pwani, kwani wenyeji walianza kushuhudia mashamba yao yakimilikiwa na watu wasiotoka maeneo hayo kuanzia enzi za jadi.
Mvurya naye amemtaka Seneta Boy kukoma kuulumbikizia kashfa muungano wa Jubilee.
Aidha, amewata viongozi wa Kwale kuendeleza kazi ya kuwahudumia wananchi badala ya kupotosha wakaazi kwa propaganda ambazo hazina ukweli wowote.
“Wakaazi wa Kwale wanamahitaji mengi ambayo yanapaswa kutekelezwa na viongozi kama vile tatizo la baa la njaa na uhaba wa maji, yanayoendelea kukumba eneo hili,” alisema Mvurya.
Haya yanajiri baada ya Seneta Boy kudai kuwa Gavana Mvurya alinadi vipande vya ardhi kwa viongozi wa muungano wa Jubilee.