Baada ya tume ya maadili na kupambana na ufisadi nchini EACC, kutoa ripoti yake ya orodha za kaunti fisadi nchini, sasa ripoti hiyo imekashifiwa vikali na baadhi ya viongozi nchini kuwa haijazingatia viegezo muhimu vya kuchunguza ufisadi nchini.
Naibu Mwenyekiti wa baraza la magavana nchini Salim Mvurya amesema kuwa tume hiyo imefanya utafiti wao bila ya kuwahusisha maafisa wa kaunti hizo hasa wakuu wa serikali za kaunti bali wahusisha baadhi ya wakaazi bila ya kufahamu kuwa wengi wao hawatoki kaunti hizo.
Murya ambaye pia ni Gavana wa kaunti ya Kwale amesema kuwa madai ya kuwa kaunti ya Kwale ndio inayoongoza kwa kashfa za ufisadi eneo la Pwani ikifwatiwa na kaunti ya Garissa na Lamu hayana ukweli wowote.
"Ripoti iliyotolewa na tume ya EACC kamwe haijazingatia viegezo mihumu vya kuchunguza kaunti zilizofisadi bali utafiti wao waliuliza baadhi ya watu ambao hata wengine sio wakaazi wa Kwale hilo sisi tunalishangaa ripoti hiyo sisi hatuwezi iunga mkono bali ni ripoti ya kugonganisha Wakenya," alisema Mvurya siku ya Jumatano kwenye mkutano na wanahabari.
Kauli ya kiongozi huyo imejiri baada ya tume ya EACC kutoa orodha ya kaunti fisadi nchini iliyosomwa na mwenyekiti wa tume hiyo Philip Kinisu na kupingwa na baadhi ya magavana nchini, licha hatua ya tume hiyo kukabiliana na kashfa za ufisadi kukumbwa na changamoto.
Sasa huenda mgogoro wa kashfa za ufisadi katika kaunti ya Kwale ukazuka upya baada ya kaunti hiyo kuhusishwa katika orodha ya kaunti fisadi zaidi eneo la Pwani.