Mgombea wa kiti cha ugavana Kaunti ya Mombasa Anania Mwaboza amekashifu hatua ya liwali wa jamii ya Sultan kuwataka wakaazi wanaoishi katika mtaa wa Mwembe Kuku, Mvita, kuondoka katika ardhi hiyo.
Akiongea na wanahabari mjini Mombasa, Mwaboza alisema hatua hiyo ni ya unyanyasaji miongoni mwa wakaazi hao, kwani wengi wao ni wazawa wa eneo hilo.
“Hatua ya kuwataka wakaazi hao kulipa kima cha shilingi zaidi ya milioni nane kwa mabwanyenye hao haitaruhusiwa kamwe,” alisema Mwaboza.
Mwaboza, ambaye ni mbunge wa zamani wa Mvita, alisema anasikitishwa na jinsi wageni wanavyodai umiliki wa ardhi hiyo.
Aliwashutumu baadhi ya viongozi wanaodaiwa kushirikiana na wageni hao kunyakua ardhi katika Kaunti ya Mombasa.
Kwa upande wake, mwenyekiti wa chama cha Jubilee tawi la Mombasa Ali Mwatsahu aliwaonya maliwali hao, na kusema kuwa mkono wa sheria utawakabili vilivyo.