Mbunge wa Msambweni Suleiman Dori amemkashifu Mbunge wa Likoni Masoud Mwahima kwa kile alichokitaja kama kuwasaliti wakaazi kwa kujiunga na chama cha Jubilee.
Amewataka wakaazi wa Likoni kumchunguza Mwahima na ikiwezekana kutompigia kura kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.
Akizungumza kwenye hafla ya kuchangisha pesa katika Shule ya wasichana ya Mtongwe, Dori alisema ni jambo la kusikitisha kuona kwamba Mwahima aliyekuwa mstari wa mbele katika kupigia debe chama cha ODM, sasa amejiunga na mrengo wa Jubilee, ambao ameutaja kama jipu kwa wakaazi wa Pwani.
Bwana Dori aliwataka wenyeji wa eneo bunge hilo kutompigia kura Mwahima kutokana na 'aibu' aliyoipa chama cha ODM katika eneo la Pwani, ambalo linafahamika kama nguzo ya chama hicho.
Mbunge wa Matuga Bwana Hassan Mwanyoha aliunga mkono usemi huo na kudai kuwa wabunge waliohamia chama cha Jubilee walifanya hivyo baada ya kupokea 'bahasha'.
Aidha, Dori aliwataka wakaazi wa Likoni kutokubali kudanganywa kuwa serikali ya Jubilee ndiyo iliwasaidia kupata hatimiliki za shamba la Waitiki, kwa kusema kuwa hiyo ilikuwa ni haki yao.
Haya yanajiri baada ya Mbunge wa Likoni Masoud Mwahima kutangaza kuhamia chama cha Jubilee.