Mbunge wa Likoni Masoud Mwahima amelalamikia ongezeko la visa vya wakaazi kuibiwa mali yao mchana, na hata wengine kuporwa hasa kwenye kivuko cha feri cha Likoni.
Akizungumza baada ya kikao na wazee wa mtaa katika afisi yake, Mwahima alisema kuwa sharti usalama wa mwananchi uimarishwe hasaa wakati huu ambapo shule zinaelekea kwenye likizo ndefu.
Mwahima alitoa mfano wa kisa kimoja ambapo mwili wa mwanafunzi wa shule ya upili ulipatikana ukielea kando ya ufuo wa bahari.
Alisema kuwa afisi yake katu haitakubali mambo kama hayo kutokea, ilhali kuna idara husika ambayo jukumu lake ni kuhakikisha kuwa mwananchi anapata usalama wa kutosha.
Aidha, amewaomba wazee wa mitaa kushirikiana na maafisa wa polisi katika kutoa taarifa zinazohusiana na maswala ya usalama.
Haya yanajiri baada ya kuzuka madai kwamba baadhi ya wazee hao hushirikiana na makundi ya vijana wanaotekeleza uovu kwenye fukwe za bahari hindi, kama njia mojawapo ya kujipatia riziki.
Mwahima alikashifu hatua hiyo na kusema kuwa wazee hao wanaojihusisha na visa vya uhalifu watakabiliwa kwa mujibu wa sheria.