Idara ya usalama imemtaka Mbunge wa Likoni Masoud Mwahima kufika katika kituo cha polisi cha Likoni kuandikisha taarifa kuhusiana na kushambuliwa kwa kituo hicho na wahudumu wa pikipiki siku ya Jumanne, wiki jana.
Taarifa kutoka kwa idara ya polisi zinasema kuwa zaidi ya wahudumu 300 wa bodaboda walikishambulia kituo hicho na kumuacha afisa mmoja na majeraha.
Akithibitisha hayo, afisa mkuu wa idara ya upelelezi eneo bunge la Likoni David Siele, amesema walimpa mbunge huyo makataa ya kati ya siku ya Ijumaa wiki jana na Jumamosi kuandikisha taarifa, ila akakiuka agizo hilo.
Siele alisema kuwa juhudi za kuwasiliana na mbunge huyo ziligonga mwamba jambo alilosema limepelekea idara hiyo kuchukua hatua nyengine dhidi ya mbunge huyo.
Kamishna wa kaunti ya Mombasa Maalim Mohammed kwa upande wake amewataka maafisa wa polisi kuwachukulia hatua kali za kisheria wote waliohusika katika uvamizi huo, huku akimtaka kiongozi wa upelelezi kutopoteza muda wa kukabiliana na watu aina hiyo.