Aliyekuwa mbunge wa Likoni Masoud Mwahima katika hafla ya awali.[Picha/ barakafm.org]
Aliyekuwa mbunge wa Likoni Masoud Mwahima ameiambia mahakama kuwa mawakala wake walizuiliwa nje ya vituo vya kupigia kura katika uchaguzi wa Agosti 8.Mwahima alikuwa akitoa ushahidi wake katika kesi ya kupinga ushindi wa Mbunge wa Likoni Mishi Mbiko.“Uchaguzi eneo la Likoni haukuwa wa haki bali ulikumbwa na wizi wa kura,” alisema Mwahima.Akitoa ushahidi wake mbele ya Jaji Erick Ogola siku ya Jumatatu, Mwahima alisema kuwa fomu 35A hazikutiwa saini na mawakala wa Jubilee kwa kuwa walizuiliwa kuingia katika vituo vya kupigia kura.Mwahima alidai kuwa mawakala waliohusika katika uchaguzi huo wa ubunge eneo la Likoni walikuwa bandia na wala sio wa chama cha Jubilee.“Mawakala waliotumika kusimamia kura hawakuwa wa Jubilee wala siwajui kamwe. Hao ni mawakala bandia na walifanywa kuokotwa mitaani,” alisema Mwahima.Aidha, mwanasiasa huyo aliongeza kuwa hakukuwa na umeme katika kituo kikuu cha kujumuisha kura cha Likoni School for the blind.“Hakukuwa na umeme na iliwalazimu maafisa wa IEBC kutumia mwangaza wa simu kujumuisha kura hizo. Ni wazi kuwa kulishuhudiwa wizi wa kura,” alisema Mwahima.Mbunge huyo wa zamani ameitaka mahakama kufutilia mbali ushindi wa Mboko na kuagiza uchaguzi huo kufanyika upya.