Mbunge wa Likoni Masoud Mwahima amewarai wakaazi wa eneo bunge lake kujiunga na chama cha Jubilee kabla ya uchaguzi mkuu ujao.
Akizungumza katika eneo la Likoni siku ya Jumatatu, katika mkutano wa wanawake, Mwahima aliwahimiza wakaazi wa eneo hilo kuhakikisha kuwa wanajitolea kikamilifu kufanya kazi na chama cha Jubilee.
Aidha, alisema kuwa iwapo wakaazi watajiunga na Jubilee na kuwachangua viongozi wa chama hicho, basi miradi mingi ya kimaendeleo itatakelezwa bila ya kuegemea upande wowote.
Mwahima alisema kuwa kama kiongozi mkongwe wa kisiasa, atahakikisha kuwa eneo bunge la Likoni limebadilika kimaendeleo, sawia na kuwaanzishia wanawake na vijana wa eneo hilo miradi mbalimbali.
“Kama mbunge mkongwe katika siasa nitahakikisha kuwa wanawake na vijana wamefaidika na miradi mbalimbali ya kimaendeleo na kujitolea kufanya kazi na chama cha Jubilee,” alisema Mwahima.
Wakati huo huo, alikikosoa chama cha ODM kwa kile alichokitaja kama ubaguzi, hasa wakati wa ugavi wa nafasi za ajira.