Mwanasiasa Suleiman Shakombo amemkosoa Mbunge wa Likoni Masoud Mwahima kwa madai ya kushindwa kuwajibikia miradi ya maendeleo katika eneo hilo.
Shakombo, aliyetangaza azma yake ya kuwania nafasi ya ubunge katika eneo hilo, alisema uongozi wa busara na maendeleo ndio unaohitajika katika jamii.
Akiongea katika mtaa wa Bofu eneo la Likoni siku ya Ijumaa, mwanasiasa huyo aliwataka wakaazi wa eneo bunge la Likoni na Kaunti ya Mombasa kwa jumla kujitenga na siasa za ubinafsi.
“Ningeomba wakaazi wa Likoni kuhakikisha kuwa wanajitenga na viongozi wa kisiasa walio na malengo binafsi, na badala yake kuwachagua viongozi waadilifu wanaojali maslahi yao,” alisema Shakombo.
Alisema kuwa ni wakati wa wakaazi wa Likoni kufanya uamuzi wa busara kabla ya uchaguzi ujao ili wapate viongozi waadilifu.
“Huyu mbunge wenu ameshindwa kuwafanyia mambo muhimu hivyo munastahili kuwachagua viongozi watakaofanya kazi,” alisema Shakombo.