Mbunge wa Likoni Masoud Mwahima ameshikilia msimamo wake wa kuunga mkono serikali ya Jubilee, licha ya shtuma anazopata kutoka kwa wanasiasa katika eneo hilo la Pwani.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mwahima ameema alichukua hatua hiyo kutokana na imani aliyonayo kwa Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake Wiliam Ruto, katika kuleta maendeleo hasa kwa wakaazi wa Pwani.

Akiongea siku ya Jumapili huko Likoni, Mwahima alitoa mfano wa hati miliki zilizotolewa na Rais Kenyatta kwa maskwota wa Shamba la Waitiki mapema mwaka huu.

“Kuna watu wanaojaribu kuharibu na kusema eti tuliuziwa shamba. Mimi nasema hatukuziwa shamba hilo bali tulipewa bure kwa kuwa shilingi elfu moja sio pesa nyingi,” alisema Mwahima.

Mbunge huyo alisema ana imani kuwa ushirikiano wake na serikali ya Jubilee utahakikisha kuwa wakaazi wa eneo hilo la Likoni wanafaidi mambo mengi ya kimaendeleo.

Wakati huo huo, Mwahima alimshukuru Seneta wa Nairobi Mike Sonko kutokana na ahadi yake ya kugharamia matibabu ya waathiriwa wa shambulizi la kanisa katika eneo hilo.

“Huu msaada wako seneta ni mkubwa sana.Wewe umetoka Nairobi lakini umesaidia watu wa hapa Likoni,” aliongeza Mwahima.

Kauli ya mbunge huyo inakuja huku kukiwa na shutuma kutoka kwa baadhi ya wanasiasa katika kanda ya Pwani dhidi ya wale walioasi muungano wa CORD na kujiunga na Jubilee.

Mwahima hata hivyo alisema maneno ya wanasiasa hao sio tishio kwake na kuwasihi wakaazi wa Likoni kumpigia kura mwaka wa 2017 kupitia chama kipya cha JAP.