Mbunge wa Likoni Masoud Mwahima amesema ana imani kuwa wakaazi wa Likoni watampigia kura katika uchaguzi mkuu ujao.

Share news tips with us here at Hivisasa

Amewataka wapinzani wake kujitayarisha kushindwa, huku akisema kuwa miradi aliyotekeleza katika eneo bunge hilo pamoja na hakikisho alilopata kutoka kwa wakaazi, ni ishara kuwa ataibuka mshindi mwaka wa 2017.

Mwahima ambaye hivi majuzi aliuasi mrengo wa Cord, amesema hawezi kutishiwa na wanasiasa wanaoanza safari yao ya kiasiasa, na kuongeza kuwa bado hawajatoshea kupambana naye kwenye kinyang’anyiro hicho.

Alisema hatua ya Baraza la mji wa Mombasa kusema litamteua atakayepambana naye haijaleta hasara yoyote kwake, kwani sera alizowaahidi wananchi anaendelea kuzishughulikia, na huenda zikakamilika kabla ya mwaka ujao.

Akizungumza na waandishi wa habari katika shule moja huko Likoni siku ya Alhamisi, Mwahima alisema kile anachojua kufikia sasa ni kwamba bado hajapata mpinzani wa kutatanisha.

“Bado wananchi wanahitaji uongozi wangu kwa manufaa ya jamii zote zinazoishi eneo hili,” alisema Mwahima.

Aidha, amekitaka chama cha ODM kukoma kumshtumu kila mara kwa hatua yake ya kuhamia mrengo wa Jubilee.

“Kila kiongozi huhamia pale anapohisi wananchi wake watanufaika. Tangu nijiunge na ODM, hakuna hata msaada ambao chama hicho kimeweza kutekeleza kwa wakaazi wa Likoni,” alisema Mwahima.