Mwakilishi wa Wadi ya Bosamaro amelalamikia hali mbaya ya barabara ya Kebirigo-Bosiango na Nyakoria.
Boniface Ombori alisema kuwa mwanakandarasi aliyepewa kazi ya kukarabati barabara hiyo bado hajaikamilisha tangu mwaka wa 2013.
Akihutubia wanahabari nje ya jengo la bunge la kaunti ya Nyamira siku ya Jumanne, Ombori alisema hali mbaya ya barabara hiyo imewaathiri wakulima wa majani chai ambao hupata wakati mgumu kusafirisha mazao yao hadi viwanda vya Nyansiongo na Kebirigo.
"Wakulima watawezaje kusafirisha mazao yao hadi kwenye viwanda vya kusaga chai kule Kebirigo na Nyansiongo ikiwa barabara hiyo haipitiki?" aliuliza Ombori.
Ombori aidha alisema kamati ya barabara kwenye bunge la Kaunti ya Nyamira yafaa kushughulikia suala hilo kwa haraka ili kuhakikisha kuwa hali ya barabara hiyo imerekebishwa.
"Kamati ya barabara yafaa kutatua shida hii kwa haraka ili kuhakikisha kuwa barabara hiyo imekarabatiwa na kuwawezesha wenyeji kusafirisha mazao yao hadi sokoni na viwanda vya kusaga chai," alisema Ombori.
Mwakilishi wadi ya Bogichora Beautah Omanga alisema kuwa yafaa bunge la kaunti hiyo limwagize mwanakandarasi aliyepewa kazi yakuikarabati barabara hiyo kujiwasilisha mbele ya bunge hilo ili kuelezea sababu yakutokamilika kwa ukarabati huo.