Kamati ya utekelezaji katika bunge la Kaunti ya Nyamira imeagizwa kuchunguza upya matumizi mabaya ya shillingi millioni 2.8 na serikali ya kaunti hiyo.
Akihutubu kwenye bunge hilo siku ya Jumanne, kiongozi wa wachache bungeni Jackson Mogusu alisema kuwa anashangazwa na ni vipi serikali ya kaunti ya Nyamira inaweza tumia shillingi millioni 2.8 kununulia maafisa wake sukari, maziwa na soda.
"Bwana spika inashangaza kwamba sukari kilo moja ambayo tunainua madukani kwa shillingi mia moja ishirini inaweza nunuliwa kwa shillingi mia tatu na hamna hatua ambayo imechukuliea hadi sasa, hata baada ya vyombo vya habari kuweka bayana ufisadi unaoendelea kwenye serikali ya kaunti hii,” alisema Mogusu.
Mwakilishi huyo wa wadi ya Nyansiongo alisema kuwa wakazi wa kaunti hiyo wamepoteza imani na serikali zilizo gatuliwa ikizingatiwa kwamba visa vya ufisadi vinaendelea kukithiri kwenye idara mbalimbali za serikali ya kaunti ya Nyamira.
"Huu sio wakati wa kwanza kwa visa vya ufisadi kuripotiwa huku Nyamira. Bado kuna utata wa lango kuu la hospitali kujengwa kwa shillingi millioni saba na pia swala tata la upanzi wa maua na kwasababu hiyo, tungependa kupata mwafaka kutoka kwako bwana spika." alisema Mogusu.
Spika wa bunge hilo Joash Nyamoko alimwagiza mwenyekiti wa kamati ya utekelezaji bungeni Ezra Mochiemo kuchunguza swala hilo nakuwasilisha ripoti mwafaka kwenye bunge hilo kwa wiki tatu zijazo.
"Hilo ni swala linaloibua hisia mseto miongoni mwa wananchi na ninamwagiza mwenyekiti wa kamati ya utekelezaji kwenye bunge hili Ezra Mochiemo na kamati yake kuchunguza madai hayo nakuwasilisha ripoti mwafaka kuhusiana na tuhuma za ufisadi humu bungeni,” alisema Nyamoko.