Mwakilishi wa kina mama katika kaunti ya Nyamira Alice Chae amshtumu vikali vitendo ambapo wanaume huwanajisi watoto wa kike na kisha kuwaua. 

Share news tips with us here at Hivisasa

Kwenye mahojiano kwa njia ya simu, Chae alisema kwamba serikali inafaa kuchunguza na kuwachukulia hatua wahusika wanaojihusisha na visa vya ubakaji wa watoto. 

"Kwa kweli hivi visa vya wanaume kuwabaka wanawake hasa watoto wasichana na kuwaua bila hatia ni makosa makubwa na serikali inafaa kuchunguza na kuwachukulia hatua kali wahusika," alisema Chae. 

Chae aidha aliwataka maafisa wa utawala hasa machifu na manaibu wao kushirikiana na wazazi ili kuripoti visa vya watu wanajihusisha na unajisi ili hatua zichukuliwe dhidi yao. 

"Kuna visa vingi vya unajisi vinavyoendelea vijijini ila haviripotiwi, na ni himizo langu kwa machifu na manaibu wao kushirikiana kuhakikisha kuwa visa hivyo vinaripotiwa ili hatua kuchukuliwa dhidi ya wahusika," aliongezea Chae. 

Haya yanajiri baada ya mtoto msichana wa umri wa miaka 12 kunajisiwa na kisha kuuawa na watu wasiojulikana huko Ndaragwa.