Mwakilishi wa Wadi ya Kabazi katika Kaunti ya Nakuru Waithaka Mwangi na Wakaazi wa Wadi hiyo wameitaka Serikali ya Kaunti hiyo kuharakisha utoaji wa pesa za Basari kwa wanafunzi.
Mwangi alisema uchelewashaji huo umewavunja wazazi moyo kuona walijaza fomu za kuomba msaada huo wa masomo miezi mitatu iliyopita na sasa wanafunzi wameenda likizoni wakiwa bado hawajapokea msaada huo.
Akizungumza siku ya Jumatano katika kituo cha kibiashara cha Kabazi, Mwakilishi huyo alisema, “Wazazi wanaona ofisi za Wawakilishi wa Wadi kama zinazochelewesha utoaji wa fedha ya Basari, ilhali fomu hizo tayari tulizirejesha katika ofisi husika baada ya wazazi kuzirejesha. Hatuelewi ni kwa nini hazijaweza kushughulikiwa.”
Wazazi hao walisema walijaza fomu za kuomba msaada huo wa masomo kabla ya muhula wa kwanza na watoto wao wamekuwa wakitatizika baada ya kufukuzwa Shuleni kufutia ukosefu wa karo.
Haya yanajiri wakati wazazi katika Kaunti Ndogo ya Subukia wakilalamikia ucheleweshaji wa Basari hizo.
“Nimekuwa na matatizo ya kumlipia mwanangu karo muhula uliopita. Alifukuzwa Shuleni mara mbili. Namuomba Gavana wetu Kinuthia Mbugua ahakikishe pesa hizo zimetolewa kwa Shule kabla ya muhula wa pili kuanza ili masomo ya watoto wetu yasihitilafishwe,” alisema Jane Wangari, mzazi kutoka Kabazi.
Naye Rael Njoroge alipendekeza utoaji wa Basari uchukue muundo wa hazina ya ustawi wa maendeleo ya maeneo Bunge kama njia moja ya kuzuia ucheleweshaji wake.
Serikali ya Kaunti imetenga Shilingi milioni moja kwa kila Wadi ambazo zinatolewa kwa wanafunzi kama Basari.