Mwakilishi wa Wadi ya Kabonyo katika Bunge la Kaunti ya Kisumu Charles Aguka amewataka wakaazi wa eneo hilo analowakilisha kuwa wavumilivu akiwahakikishia kwamba miradi yote aliyowaahidi itaafikiwa kabla ya kipindi chake kumalizika.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akihutubu siku ya Jumamosi katika soko la Cherwa alikokutana na wafuasi wake ambao walilalamikia hali mbovu ya barabara za eneo hilo, Aguka alisema kwamba miradi yote iliyopendekezwa ikiwemo ukarabati wa barabara za eneo hilo itatimizwa hata kama itakawia kutokana na utaratibu wa usambazaji wa pesa za Kaunti mashinani.

“Mnaelewa ya kwamba pesa za Serikali siyo zangu binafsi na lazima zitolewe kwa utaratibu uliowekwa kwa mujibu wa sheria na wala siyo mimi mwenye kuamrisha. Kwa hiyo nawaomba tu kufuatiana na sheria na mamlaka niliyopewa,” alisema Mwakilishi Aguko.

Aidha, Aguka aliahidi kutekeleza miradi zaidi katika kipindi cha matumizi ya pesa za Serikali kwenye bajeti ijayo ili kuwaridhisha wakaazi wa eneo hilo analowakilisha kwenye Bunge la Kaunti.

“Mlinipatia kura kwa hivyo nilazima niwatumikie hata katika hali ngumu kiasi gani. Nitahakikisha kwamba mnapata kufaidika kwenye msimu huu wa Serikali ya ugatuzi kwa kuwaletea maendeleo mengi mashinani.” Aliongeza Aguko.

Pia alisema kuwa amejiunga na wenzake kuunga mkono ajenda ya Magavana kushinikiza Serikali Kuu kuongeza mgao wa pesa za Kaunti, maarufu Pesa Mashinani ili kuwapa wananchi wa Kenya huduma bora zaidi.

Wakaazi katika maeneo ya Cherwa, Kabonyo na Kadongo walilalamikia vikali hali ya barabara za eneo hilo wakisema kuwa hazipitiki haswa wakati huu wa mvua, ambapo vijana wengi katika eneo hilo hutegemea biashara ya uchukuzi wa Bodaboda.