Mwakilishi wa Wadi ya Kiamokama ilioko katika eneo Bunge la Nyaribari Masaba, Kennedy Mainya amewapa changamoto wanafunzi kutia bidii masomoni ili wajisaidie katika siku zijazo.
Mwakilishi huyo pia amewaomba wazazi kutuma maombi ya fedha za ustawi wa Wadi ili kuwasaidia watoto wao kuendelea na masomo.
Akizungumza siku ya Jumatatu katika shule ya Upili ya Mobamba iloko katika Wadi yake kwenye hafla ya kepeana zawadi kwa wanafunzi waliofanya vyema katika mtihani wa kitaifa wa mwaka jana, Mainya alisema wengi wa wale wanaofaa kutuma maombi ya usaidizi wa fedha hizo hawakutuma na hivyo kuwaomba kutuma ili wanao waweze kunufaika na mpango wa ufadhili huo wa Serikali ya Kaunti ya Kisii.
“Ninawaomba wazazi kutuma maombi ya pesa za Ward Development Fund kuwasaidia watoto wao ili waweze kupata pesa hizo kugharamia masomo yao. Aidha, changamoto kuu tunayokumbana nayo ni kuwa wanaojiweza ndio wanatuma maombi ilhali mpango huu unapaswa kuwafadhili wasiojiweza katika jamii,” alisema Mainya.
Kwa upande wake, Gavana wa Kaunti ya Kisii James Ongwae ambaye pia alihudhuria hiyo mkutano wa kupeana zawadi, aliwaomba wazazi kutoka Kisii kukumbatia mpango huo kwani unalenga kuhakikisha wanafunzi kutoka familia maskini wanaendelea na masomo yao.
Gavana Ongwae aliahidi kuongeza fedha hizo kutoka milioni tatu katika mwaka huu wa matumizi hadi milioni tano katika bajeti ya mwaka ujao ili kuwasaidia wanafunzi wengi wanaoonekana kuwa na mahitaji ya usaidizi.