Mwakilishi wa wanawake katika Kaunti ya Kwale Zainab Chidzuga ameitaka idara ya trafiki kuyakamata magari yanayotoka Tanzania, kwa madai ya kukiuka sheria za barabarani.
Chidzuga alidai kuwa magari hayo yamesababisha ajali nyingi hasaa katika maeneo ya Likoni na Lungalunga.
Akihutubia wakaazi katika hafla ya mazishi ya jamaa mmoja aliyefariki kwenye ajali ya barabarani katika eneo la Kanana huko Shimoni, Chidzuga alidai kuwa magari hayo ya mizigo kutoka Tanzania huendeshwa kwa mwendo wa kasi, hali inayosababisha maafa mengi.
Kiongozi huyo wa wanawake alitoa mfano wa basi la kampuni ya Smart lililotumbukia baharini katika Kivuko cha feri cha Likoni.
Alisema kuwa ajali hiyo ilitokea kutokana na ukiukaji wa sheria za trafiki.
Aidha, alidai kuwa wengi wa madereva kutoka Tanzania huwa wanakiuka sheria za barabarani hali aliyosema huchangia ongezeko la ajali za barabarani.
Ameitaka mamlaka ya barabara kuu nchini KENHA kufanyia upanuzi barabara kuu ya Mombasa-Lungalunga ili kudhibiti mikasa ya ajali.
Kufikia sasa watu 10 wameaga dunia kutokana na ajali zilizoshuhudiwa katika barabara hiyo.