Kufuatia hatua ya serikali ya kitaifa kupitia kwa wizara ya usalama kupunguza idadi ya walinzi wanaomlinda gavana wa kaunti ya Mombasa Hassan Joho na kisha kumuamuru kurejesha bastola yake, sasa mwakilishi wa walio wengi katika bunge la kaunti ya Nyamira Raban Masira amejitokeza kushtumu vikali hatua hiyo. 

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Akihutubu kwenye hafla moja ya mazishi kule Egesieri siku ya Jumapili, Masira alisema kuwa agizo la serikali kuu kumwagiza Gavana Joho kurejesha bastola yake na hata pia kumpunguzia idadi ya walinzi ni dhuluma kwa uongozi wa ugavana nchini. 

"Tuna aina mbili za serikali humu nchini zikiwemo ya kitaifa na ile ya Kaunti, na kwa sababu Gavana Joho ni kiongozi wa serikali ya jimbo la Mombasa, sharti aheshimiwe, na ndio maana kwamba hatua ya serikali kumpunguzia idadi ya walinzi wake na hata kumuagiza kurejesha bastola yake kwa serikali ni dharau kubwa kwa cheo cha ugavana," alisema Masira.

Masira aidha aliongeza kusema kuwa agizo hilo la serikali ni njia mojawapo ya mikakati serikali ya Jubilee imeweka ili kuwasahaulisha wakenya kuhusiana na sakata ya uvujaji wa mamillioni ya pesa kutoka kwa hazina ya shirika la kitaifa la huduma kwa vijana nchini NYS. 

"Hali hii ya serikali kuanza kumhangaisha gavana Joho ni mbinu serikali ya Jubilee inatumia ili kuwasahaulisha wakenya kutoka na sakata ya shirika la NYS, na huu ni mpango wa kuwapumbaza wakenya dharua ambalo kamwe hatutalikubali," aliongezea Masira. 

Picha: Mwakilishi wa walio wengi katika bunge la kaunti ya Nyamira Raban Masira. Amekashfu hatua ya serikali kumpkonya Gavana wa Mombasa walinzi wake. WMAINA/Hivisasa.com