Mwakilishi wa wadi ya Bonyamatuta katika kaunti ya Nyamira Robinson Mocheche amekashifiwa kwa kugeuza mradi wa Kalindi cha vijana na kuwa wake binafsi.
Kulingana na Janet Kwamboka, ambaye ni mweka hazina wa chama hicho cha Umoja Youth Group kilichoko katika wadi hiyo, mwakilishi huyo aliwaahidi kuwasaidia kuanzisha mradi wa ukulima wa 'greenhouse' ambayo aliwasaidia kupata, lakini baadaye akatumia baadhi ya viongozi wa kikundi hicho ambao walimuuzia greenhouse hiyo kabla haijatumika.
"Tumeshangaa kugundua kwamba greenhouse yetu ambayo tumetumika kutia sahii imechukuliwa na kiongozi ambaye tulidhania anatusaidia kujiendeleza," alisema Kwamboka.
Aidha, vijana hao wamemkashfu kiongozi huyo kwa kuwatumia viongozi hao kuwanyanyasa kwa manufaa yake binafsi.
"serikali inajua kikundi hiki kimefaidika kupitia mradi huu kumbe inamfaidi kiongozi," aliongeza mmoja wa wanachama hao.
Inasemekana kuwa Mocheche ana miradi hiyo ya ukulima wa greenhouse mbili ambayo inasemekana amepokea kwa njia hiyo ya ujanja wa kusaidia vikundi vya vijana.
Hata hivyo mbunge huyo hakukataa wala kukubali madai hayo ila tu kusisitiza kuwa atakutana na vijana hao kusuluhisha shida hiyo.