Mwakilishi wa eneo wadi ya Nyamaiya Laban Masira amejitokeza kupinga vikali mpango wa serikali ya kaunti ya Nyamira kutaka kujenga vijiduka 80 katika soko la Keroka na vingine 50 kwenye soko la Kebirigo kwenye mwaka wa kifedha wa 2016- 2017.
Akichangia kwenye hoja ya kutaka kuidhinisha mswada wa mpango wa miradi ya uwekezaji katika bunge la kaunti hiyo siku ya Jumanne, Masira alishangazwa na ni kwa nini miji hiyo miwili iwe ndiyo tu itakayojengewa vijiduka hivyo ikizingatiwa kwamba kuna baadhi ya miji kwenye kaunti hiyo zilizo na mahitaji sawia.
"Isiwe kwamba maeneo ya Kebirigo na Keroka ndiyo pekee yatakayojengewa vioski ilhali kuna miji mingine Nyamira ambayo pia ina mahitaji ya vioski," alisema Masira.
Masira aidha aliongeza kwa kuitaka kamati ya fedha na uwekezaji kwenye bunge hilo kudadisi na kubaini maeneo yaliyo na mahitaji zaidi ya miradi ya maendeleo ili yaongezewe fedha zaidi.
"Ni ombi langu kwa kamati ya fedha na uwekezaji kwenye bunge hili kudadisi ili kubaini mahitaji ya maeneo wadi mbalimbali kabla yakupokeza fedha zakufadhili miradi kwenye maeneo hayo," liongezea Masira.