Mwakilishi wa Wadi ya Gesima Ken Atuti, ameshtumu hatua ya kuvunjwa kwa vyama tanzu vya muungano wa Jubilee.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza alipo fanya kikao na vijana siku ya Jumatatu, Atuti alimsihi kinara wa chama cha URP, Naibu wa Rais William Ruto kutokubali pendekezo hilo lakuvunjilia mbali vyama tanzu vya jubilee kwa kuwa iwapo hilo litafanyika, huenda chama hicho cha URP kikapoteza umaarufu wake mashinani.

"Sio mimi tu ninayepinga pendekezo la kuvunjiliwa mbali vyama tanzu vya muungano wa Jubilee. Tuko wengi lakini ni ile viongozi wengine wanaogopa kuzungumzia swala hilo.Iwapo chama cha URP kitavunjwa, basi huenda ikawa vigumu kwa naibu rais kuwashawishi wapiga kura hasa mashinani kumpigia kura za urais ifikapo mwaka wa 2022, na kwasababu hiyo, tungeomba tuendelee kuwa washirika kwenye muungano wa Jubilee," alisema Atuti.

Atuti aidha alisema kuwa iwapo chama cha URP hakitavunjiliwa mbali, basi itakuwa rahisi kwa Naibu wa Rais William Ruto kujipima nguvu na mahasimu wake wa kisiasa mbele ya uchaguzi wa mwaka wa 2022.

"Unapokuwa na chama chako cha kisiasa huwa rahisi kwa watu kukufahamu vizuri kwa kuwa chama kitakuwa msingi wakung'ang'ania kiti cha urais. Iwapo hilo halitazingatiwa, huenda ndoto ya William Ruto kuliongoza taifa hili ikadidimia,” alisema Atuti.

Atuti alisema kuwa amepanga kukutana na Naibu Rais William Ruto mapema mwezi Novemba ili kuzungumzia swala hilo.

"Tayari mimi na wenzangu tushawasiliana na afisi ya Ruto na tumeahidiwa kukutana naye mapema mwezi ujao ili tumwambie ukweli kuhusiana na swala hili tata,” alisema Atuti.