Mwakilishi wa Wadi ya Kongowea Jabes Oduor, amemuandikia barua Spika wa Bunge la Kaunti ya Mombasa Thadius Rajwayi, akitaka mshahara wake upunguzwe kwa asilimia 50 kuanzia mwezi Mei mwaka huu.

Share news tips with us here at Hivisasa

Katika barua hiyo iliyotumwa kwa wanawahabari siku ya Jumamosi, Oduor alisema anataka mshahara wake upunguzwe sambamba na marupurupu yake katika kipindi kilichosalia kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.

Barua hiyo ilieleza kuwa Oduor alichukua hatua hiyo ili kuwasaidia watoto mayatima katika makaazi ya Angaza Children Centre katika eneo bunge la Nyali, pamoja na kushughulikia maswala mengine katika jamii.

Spika wa bunge hilo Thadius Rajwayi, alikiri kupokea barua hiyo na kuthibitisha kuwa matakwa ya Oduor yatazingatiwa baada ya Tume ya kutathmini mishahara na marupurupu ya wafanyikazi wa umma nchini SRC, kufahamishwa kuhusiana na uamuzi huo.

Baadhi ya wawakilishi wa bunge la Kaunti ya Mombasa waliitaja hatua hiyo kama ya kisiasa, kwani Oduor analenga kuwania kiti cha ubunge cha Nyali katika uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.