Mwakishi wadi wa Bokeira Karen Atuya amewaonya vikali wahalifu wanaowahangaisha wafanyabiashara katika eneo la Nyamusi. 

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Akihutubu kwenye hafla ya mazishi ya kumzika mmoja wa wadumisha usalama vijijini Paul Nyanumba, aliyeuwawa kwa kupigwa risasi na washukiwa wa uhalifu kule Nyamusi, Atuya aliahidi kushughulikia suala la usalama ili kuwaepusha wakazi na mashambulizi zaidi. 

"Kwa hakika kuna wahalifu ambao wamekuwa wakiwahangaisha watu wa eneo hili hasa wafanyabiashara ila ukweli ni kwamba visa hivi vinaendelea kukithiri, mimi kama mwakilishi wadi wa eneo hili nitahakikisha kwamba maafisa wa polisi wanafanya operesheni hapa hadi visa hivi vipungue," alisema Atuya. 

Atuya aidha aliwaomba wazazi kushirikiana na vyombo vya usalama ili kusaidia katika udumishaji usalama katika eneo hilo kwa kuwahimiza kuchunguza wanakotoa mali wanao wasio na ajira. 

"Sisi kama wazazi vilevile tuna jukumu la kuhakikisha kuwa usalama unadumishwa miongoni mwetu, na kwa kweli inakuwaje kwamba wewe kama mzazi unamwona mwanao akiwa na mavazi mazuri na anaishi maisha ya starehe ilhali hana kazi ama biashara na kisha ukose kujua mwanao anakotoa pesa hizo," aliongezea Atuya.