Mwakilishi wadi ya Solai, kaunti ya Nakuru Paul Chebor Kibet amewashtumu vikali wale wanaopinga muungano wa vyama vya TNA na URP.
Akizungumza Jumatano katika eneo lake, Chebor alisema kuwa kuunganishwa kwa TNA na URP ni muhimu kwa taifa.
"Mi nina hakika kwamba kuunganishwa kwa TNA na URP ni kwa manufaa ya taifa hili na wale ambao wanapinga wanajitakia makuu,"alisema Chebor.
Kwa mujibu wake, kumekuwepo na migogoro hasua katika vyama na hivyo basi kuunganishwa kwa TNA na URP kutasaidia pakubwa katika kumaliza migogoro.
Ni kutokana na jambo hilo ambapo alitoa wito kwa wakaazi wa kaunti ya Nakuru kuunga mkono kwa hatua hiyo.
"Tumekuwa tukishuhudia migogoro hata katika mabunge ya kaunti kwa sababu kuna wale wanashikilia kuwa ni wa URP na kuna wanaoshikilia ni wa TNA, hivyo basi kuunganishwa kwa vyama hivi viwili kutasaidia pakubwa katika kumaliza matatizo haya,"aliongeza Chebor.
Wakati huo huo, mwakilishi wadi huyo aliyechaguliwa kwa tiketi ya chama cha URP ametangaza kuwania kiti cha eneo bunge la Rongai katika uchaguzi mkuu ujao.
Kiti hicho kwa sasa kinashikiliwa na mbunge Raymond Moi.