Mwakilishi wa wadi ya Kiabonyoru James Sabwengi amewarahi wazazi kuwekeza pakubwa kwenye elimu ili kusaidia katika ustawishaji wa maendeleo.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akihutubia wakazi wa eneo la Egentubi siku ya Jumapili, Sabwengi alisema kuwa yafaa wazazi wahakikishe kuwa wanao wanahudhuria shule iwapo wanataka kustawi kimaendeleo. 

"Elimu ni mhimu sana kwa ustawishaji wa taifa, na iwapo tuna mipango ya kutaka kustawi, sharti tuhakikishe kuwa watoto wetu wanahudhuria shule," alisema Sabwengi. 

Sabwengi aidha aliongeza kwa kuwashukuru wakazi wa eneo la Kiabonyoru kwa kumpigia kura ili kuwawakilisha kwenye bunge la kaunti ya Nyamira, huku akiahidi kutekeleza miradi muhimu ya kustawisha eneo lake la uwakilishi kimaendeleo. 

"Ninawashukuru sana kwa kunichagua ili niwaongoze kama mwakilishi wadi wa eneo hili, na naweza kuwathibitishia kwamba nitahakikisha kuwa miradi muhimu ya maendeleo inazinduliwa chini ya uongozi wangu," aliongezea Sabwengi.