Mwakilishi wadi wa eneo la Gesima Ken Atuti amejitokeza kuwasihi wazazi na walezi wa watoto walio na upungufu wa kiakili kutowafungia wanao machumbani.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akihutubu kwenye mkutano wa hadhara kule Gesima siku ya Jumapili, Atuti alisema kuwa haifai wazazi kuwafungia machumbani watoto walio na upungufu wa kiakili kwa maana wana haki za utangamano kama watu wengine. 

"Katiba imetaja wazi kwamba kila mtu ana haki ya utangamano, na ni hatia kwa mzazi yeyote kumfungia mwanaye chumbani eti kwa sababu ana upungufu wa kiakili," alisema Atuti.

Atuti aidha aliwataka wazee wa vijiji kwa ushirikiano na machifu kutambua na kuwaripoti watu wanaokisiwa kuwafungia wanao machumbani kutokana na hali ya kuwa na upungufu wa kiakili, huku akitaja hali hiyo kama dhuluma. 

"Wazee wa vijiji na machifu ndio maafisa wanaowafahamu vyema watu wanaoishi nao vijijini, na ni ombi langu kwao kuhakikisha kwamba wanatambua wale wahusika wanaowafungia wanao machumbani ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao," aliongezea Atuti. 

Picha: Mwakilishi wadi ya Gesima Ken Atuti. Amewasihi wazazi kutowabagua wanao ambao wana upungufu wa kiakili. Maktaba