Aliyekuwa mgombea wa kiti cha ugavana Kaunti ya Kwale Chirau Mwakwere katika hafla ya awali.[Picha/ the-star.co.ke]
Aliyekuwa mgombea wa kiti cha ugavana Kaunti ya Kwale Chirau Mwakwere amesema yuko tayari kutoa ushahidi wake kwenye kesi ya kupinga ushindi wa Gavana Salim Mvurya.Akizungumza nje ya jengo la Mahakama baada ya kuhudhuria kikao cha kesi hiyo siku ya Jumatatu, Mwakwere alisema kuwa ana ushahidi wa kutosha kuonyesha kuwa ushindi wa Mvurya haukuwa wa haki.“Nimejipanga vya kutosha na niko tayari kuweka wazi jinsi wizi wa kura ulivyofanyika Kaunti ya Kwale,” alisema Mwakwere.Mwakwere alisema kuwa ana imani kuwa ushindi wa Mvurya utatupiliwa mbali na mahakakama, kutokana na ushahidi atakaoutoa mbele ya Hakimu Thande Mugure.Kesi hiyo iliwasilishwa mahakamani na mpiga kura Mwamlole Tchappu Mbwana, ambaye alidai kuwa uchaguzi huo wa ugavana ulikumbwa na visa vingi vya wizi.Mwamlole alisema yuko tayari kutoa ushahidi wake mbele ya mahakama ili kuweka wazi jinsi wizi wa kura ulivyofanyika katika vituo vya kupigia kura Kaunti ya Kwale.“Nina ushahidi wa kutosha katika kesi hii na sitalegeza kamba kamwe,” alisema Mwamlole.Kwa upande wake, Gavana Mvurya aliwasilisha ombi mahakamani ya kutaka kesi hiyo kutupiliwa mbali kwa kusema kuwa haikujumuisha jina la naibu gavana.Kupitia wakili wake William Mogaka, Mvurya ameitaka mahakama kutupilia mbali kesi hiyo kwa kusema kuwa haikutimiza vigezo muhimu vya kesi za uchaguzi.Ombi la kutaka kesi hiyo itupiliwe mbali itasikilizwa Novemba 8, 2017.