Mwalimu mmoja wa Shule ya Msingi alikana mbele ya Mahakama ya Kisumu madai kuwa alitumia stakabadhi ghushi kuonyesha kuwa mkewe amefariki ili kufidiwa na Kampuni ya bima.

Share news tips with us here at Hivisasa

Mwalimu Alfred Omondi wa Shule ya Msingi ya Akal, Kaunti ya Kisumu pia alikana kuwa kitendo chake kilitokana na hali kuwa mkewe wa pili na mtoto wake walikuwa wagonjwa na hivyo walihitaji matibabu ya dharura.

Omondi ameshtakiwa kwa kutoa habari za uongo kwa Naibu wa Chifu wa Kata Ndogo ya Ulamba, Samuel Aketch kwamba mkewe Lilian Atieno alifariki Machi 27 2012.

Anadaiwa kuomba Chifu ampe kibali cha mazishi ili kumzika mkewe. Upande wa Mashtaka uliambi Mahakama kuwa Naibu wa Chifu huyo aliyeaga dunia mwezi Juni 2014 alihadaiwa na Omondi.

Mahakama hiyo pia iliambiwa kuwa Naibu wa Chifu Aketch hakuthibitisha taarifa hizo na hivyo kupeana stakabadhi hiyo muhimu kwa mshtakiwa Omondi.

Afisa wa uchunguzi almaarufu C.I.D. Zakayo Mwangi aliambia Mahakama kuwa baada ya kupewa kibali cha mazishi, Omondi alifululiza kwenda kupewa fidia ya kifo kutoka kampuni ya Pan African Insurance mjini Kisumu.

Kabla ya kufidiwa pesa hizo, Kampuni ilifanya uchunguzi wake na ndipo ikabainika kuwa mke wa mshtakiwa hukuwa amefariki kama ilivyodaiwa na kwamba alikuwa anaendesha biashara ya saluni mjini Ugunja.

“Hamna pesa zilizotolewa na Kampuni hiyo ya bima kwani ilibainika kuwa mke wa Omondi alikuwa hai na anafanya kazi mjini Ugunja Kaunti ya Siaya,” alieleza Afisa Mwangi.

Mahakama iliamuru kuwa kesi ya mshtakiwa Omondi isikilizwe mnamo tarehe Mei 21 mwaka huu.