Mwalimu mkuu wa shule ya upili ya Marindi Benard Osumo amejitokeza kuwataka viongozi wa kisiasa katika kaunti ya Nyamira kuisadia shule hiyo kupata ardhi ili kuiwezesha kupanuliwa kwa minajili ya kukidhi mahitaji ya wanafunzi.
Akihutubu shuleni humo kwenye hafla ya kuwapokeza zawadi wanafunzi waliotia fora kwenye mtihani wa kidato cha nne mwaka jana siku ya Jumapili, Osumo alisema kuwa shule hiyo inahitaji kupata ardhi kwa minajili ya upanuzi.
"Tuna upungufu wa ardhi kwenye shule hii, ikizingatiwa kwamba idadi ya wanafunzi inaendelea kuongezeka, na ni ombi langu kwa viongozi wa kisiasa kujitokeza kutusaidia kupata ardhi ili tuweze kupanua ujenzi wa shule," alisema Osumo.
Osumo aidha aliongeza kwa kumpongeza mbunge wa eneo bunge la Mugirango magharibi kwa kujitolea kwake ili kufadhili ujenzi wa madarasa nane katika shule hiyo.
"Kwa sababu idadi ya wanafunzi inaendelea kuongezeka hata zaidi, kwa siku za hivi karibuni tumekuwa tukishuhudia misongamano ya wanafunzi madarasani ila ni afueni kwetu kwa maana mbunge wa eneo hili James Gesami ameahidi kufadhili ujenzi wa madarasa nane," aliongezea Osumo.